Historia ya sera nchini Tanzania imekuwa ni ya mabadiliko ya mara kwa mara ambayo lengo lake limekuwa ni kuongeza ufanisi na uzalishaji katika sekta muhimu za uchumi. Dokezo hili linatoa muhtasari wa kitabu kilichotokana na utafiti uliochunguza uwezo wa mabadiliko mbali mbali ya sera kuiongezea sekta ya kilimo, hususan wakulima wadogo, nguvu ya ushindani katika masoko mbali mbali ndani na nje ya Tanzania. Ushahidi utokanao na utafiti huu unaonyesha kwamba baadhi ya sera za kilimo zilizotungwa na kutekelezwa mara tu baada ya uhuru zilichangia kuzorotesha uzalishaji wa mazao ya biashara. Unaonyesha pia kwamba sera zilizolenga marekebisho ya kimuundo maarufu kama ‘structural adjustment’ na utandawazi hazikufanikiwa sana kuongeza uzalishaji kwenye kilimo kama ilivyotarajiwa. Kutokana na hilo hoja kubwa ni kwamba ili kuviondoa vikwazo hasi vya kisera kwenye mfumo wa soko vinavyopunguza ufanisi kwenye sekta ya wakulima wadogo, ni vizuri kutumia taratibu na mifumo ya kimasoko na isiyo ya kimasoko kwa uratibu mzuri wa pamoja.